Title Image

Uzinduzi wa Mradi wa Skuli Yetu ni Hazina Yetu chini ufadhili wa Milele Zanzibar Foundation

news phpto

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Ali Juma Shamuhuna akizindua madarasa katika skuli ya Mbuyu Tende wilaya ya Kaskazini ‘A’ yaliyojenga chini ya Milele Zanzibar Foundation

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ali Juma Shamuhuna amesifu juhudi zinazochukuliwa na taasisi zisizo za kiserikali katika kusaidia maendeleo ya wananchi wa Zanzibar kupitia sekta elimu kwa kuwajengea mazingira bora walimu na wanafunzi katika skuli zao.

Waziri Shamuhuna ameyasema hayo wakati alipokuwa akizindua mradi mkubwa wa ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, vyoo, kuchimba visima na vikalio kwa skuli 21 za Zanzibar mradi unaofadhiliwa na Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation huko katika skuli ya Mbuyu Tende wilaya ya Kaskazini ‘A’

Aidha ameipongeza taasisi hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutoa fursa ya wananchi na hasa wanafunzi kupata elimu bora kupitia mradi huo unaojulikana kwa Skuli Yetu ni Hazina Yetu kwa kuweka mazingira mazuri ya masomo yao.

Vile vile amebainisha nia ya Taasisi hiyo kuwajengea mazingira mazingira bora na kuwaondolea usumbufu walimu kwa kuwajengea nyumba za makaazi katika skuli wanazosomesha ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi kama inavyostahiki.

Katika uzinduzi huo waziri Shamuhuna pia amewapongeza wazee wa kijiji cha Mbuyu Tende kwa kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono kwani ameeleza kuwa hii inaonesha kujali juhudi za wadau wa maendeleo na kufahamu umuhimu wa suala la elimu kwa watoto wao.

Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation chini ya mradi wa Skuli Yetu ni Hazina Yetu itatekeleza shughuli zake hizo katika skuli 21 ambazo kwa Unguja ni Mbuyutende, Kiongwe, Kidagoni, Pangatupu, Kiboje, Mtoni Kidatu, Pagali, Bambi, Charawe, Chutama, Bandamaji na Dunga.

Kwa upande wa Pemba skuli tisa zitafaidika na mradi huo ambazo ni Mahuduthi, Micheweni, Mnarani, Minungwini, Birikau, Mkia wa Ng’ombe, Msuka, Mkanyageni na Kipangani.

Mkurugenzi wa taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Ndugu Yousuf Luiz Caires amesema mradi huo utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni Tatu ambapo taasisi yake itatoa shilingi 2,995,600,000/- sawa na asilimia 99.2 ambapo Shilingi 22,680,000/- sawa na asilimia 0.8 zitatolewa na wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Mradi huo utanufaisha zaidi ya wanafunzi 8,000 walimu 84 katika skuli hizo na pia kutoa mafunzo mbali mbali kwa walimu ili waweze kuvitumia vifaa watavyoweza kuviingiza katika skuli zao