Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa, amefanya ziara ya ndani katika Ofisi za Baraza la Mitihani la Zanzibar, huko Vuga Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ziara hiyo ambayo ilifuatiwa na mkutano mfupi na watendaji wa baraza hilo wenye lengo la kuwapongeza watendaji hao kwa kazi nzuri wanayoifanya hususan kwa kuweza kutangaza matokeo ya mwaka huu 2023 ya darasa la saba kwa wakati , jambo hilo limeweza kuwatia moyo wa imani wazazi, wanafunzi na wadau mbali mbali wa Elimu nchini .
Aidha Mhe. Lela amesema, licha ya changamoto mbali mbali zilizopo katika baraza amewashauri watendaji kuongeza nguvukazi katika baadhi seksheni hasa katika kitengo cha ICT .
Sambamba na hayo Waziri Lela amelitaka baraza kuwatumia watu wenye weledi na uzoefu wa muda mrefu kwa kuwatumia walimu husika kupima na kutathmini kwani kazi ya upimaji inahitaji uelewa thabiti kati ya mpimaji na anayepimwa katika ngazi husika.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Ndugu Mwanakhamis Adam Ameir amesema, Baraza la Mitihani ndiyo muhimili muhimu wa Wizara ya Elimu, hivyo hapana budi kwa watendaji hao wawe ni wataalamu waliobobea ili waweze kutunga mitihani yenye ubora na viwango vinavyokubalika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hilo Bw. Othman Omar Othman, kwa niaba ya watendaji wengine amesema, wamefarajika na ujio huo, hivyo wameyapokea na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote waliyopewa kwa maslahi ya taifa.