Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa ameipongeza Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha kwa muundo mzuri wa utoaji wa elimu ambao unazalisha wataalamu wenye weledi unaowezesha wahitimu kuweza kujiajiri mara baada ya kuhitimu.
Mhe. Lela amesema hayo machi 5, 2024 alipotembelea Taasisi hiyo kwa lengo la kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa ikiwa ni kuona namna ya taasisi na vyuo vya elimu ya juu nchini Tanzania vinavyojiendesha.
“Nampongeza Uongozi wa Taasisi kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya na kitu kikubwa nilichojifunza katika taasisi hii ni kujikita katika kufanya tafiti na sisi tumekuja kujifunza ili kuleta magaeuzi kupitia chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ili kuangazia taasisi zetu ambazo tunaweza kuzikita katika masuala ya tafiti ili kutatua changamoto mbalimbali za jamii” amesema Mhe.Lela
Ameongeza kuwa, taasisi hiyo imefanya vyema kwa kuanzisha Ndaki ya Biashara na Jamii ili kuwezesha wataalam wa bunifu na tafiti mbalimbali kuwa na akili ya biashara pale wanapohitimu elimu yao.
Aidha, ametoa wito kwa taasisi za elimu ya juu kujifunza kutoka katika taasisi ya Nelson Mandela ili kuwajengea uwezo na kuwawezesha wahitimu kibiashara na kidigitali kwa manufaa binafsi na jamii kwa ujumla.
Naye Makamu Mkuu wa Taasisi Prof. Maulilio Kipanyula ameahidi kuendeleza ushirikiano na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ili kukuza elimu katika fani mbalimbali ikiwemo tafiti, bunifu, sayansi na Teknolojia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya TEHAMA katika Elimu Zanzibar Bw. Mbwana Yahya Mwinyi ameeleza kufurahishwa na mipangilio ya tehama katika taasisi, hivyo kuangalia namna ya kushirikiana kwa karibu katika kukuza na kuendeleza sekta ya Elimu nchini.
Katika ziara yake Mhe. Lela amefanikiwa kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Kituo cha kisasa cha Elimu Kidigitali C-CODE), ICT Resource center na kituo Atamizi kwa ajili ya kuatamia bunifu za wanataaluma ambapo ni maeneo muhimu katika Taasisi yanayotumika kukuza bunifu za wataalamu.