Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Bi. Fatma Mabrouk Khamis amesema Maafisa Habari na Uhusiano wanadhamana ya kuonesha na kuelezea maendeleo yaliyofikiwa katika Wizara zao.
Amesema hayo kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh Lela Muhamed Mussa wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Maafisa Habari na Uhusiano wa Wizara hiyo katika ukumbi wa mikutano Chuo cha Utalii Maruhubi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema kila mmoja ana dhamana na jukumu la kutangaza habari za kimkakati zinazofanyika katika Idara zao. Amesema Maafisa hao wanatakiwa waendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuhakikisha kila habari za kuendelea kujenga sifa nzuri za taifa lao wanazitoa kwa wakati na kwa kufata sheria.
Aidha amesema mawasiliano ndio sehemu inayotegemewa na jamii kwa kupata Habari na taaluma za kila kinachofanyika nchini. Amesema upatikanaji wa habari itasaidia jamii kujua kinayofanywa na Serikali yao kwa ajili ya wananchi wake.
Aidha Katibu Fatma amesema Wizara ya Elimu ni moja kati ya Sekta mama katika Maendeleo ya Zanzibar na ni Sekta inayofanya vizuri katika Awamu hii ya Nane, hivyo Maafisa Uhusiano hawana budi kuhakikisha Maendeleo yaliiopo katika sekta elimu nchini yanatangazwa kwa maslahi ya jamii.